Yeremia nyumbani kwa mfinyanzi
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Yeremia, inuka uende nyumbani kwa mfinyanzi, na huko nitakupa maneno yangu.” 3Basi, nikateremka mpaka nyumbani kwa mfinyanzi, nikamkuta mfinyanzi akifanya kazi yake penye gurudumu la kufinyangia. 4Na ikawa kwamba chombo alichokifinyanga kilipoharibika mikononi mwake, yeye alifinyanga upya chombo kingine kadiri ilivyompendeza.
5Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: 6“Enyi Waisraeli! Je, mimi Mwenyezi-Mungu siwezi kuwafanya nyinyi kama alivyofanya mfinyanzi huyu? Jueni kuwa kama ulivyo udongo mikononi mwa mfinyanzi, ndivyo nyinyi mlivyo mikononi mwangu. 7Wakati wowote nitakapotoa tamko kuhusu taifa au ufalme kwamba nitalingoa na kulivunja na kuliangamiza, 8halafu taifa hilo likageuka na kuacha uovu wake, basi, mimi nitaacha kulitendea yale mambo niliyokusudia kulitendea. 9Hali kadhalika, wakati wowote nikitoa tamko kuhusu taifa au ufalme kwamba nitalijenga na kulistawisha, 10kisha taifa hilo likafanya uovu mbele yangu na kukataa kunitii, basi, mimi nitaacha kulitendea mema hayo niliyokusudia kulitendea. 11Sasa, basi, waambie watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi Hufinyanga jambo ovu dhidi yenu na kufanya mpango dhidi yenu. Rudini na kuacha njia zenu mbaya, mkarekebishe mienendo yenu na matendo yenu. 12Lakini wao watasema, ‘Hiyo ni bure tu! Tutafuata mipango yetu wenyewe na kila mmoja wetu atafanya kwa kiburi kadiri ya moyo wake mwovu.’”
Watu wanamkataa Mungu
13Basi, Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Yaulize mataifa yote:
Nani amewahi kusikia jambo kama hili.
Israeli amefanya jambo la kuchukiza mno.
14Je, majabali ya Lebanoni hukosa theluji?
Je, vijito vya maji vya milima yake hukauka?18:14 aya hii Kiebrania si dhahiri.
15Lakini watu wangu wamenisahau mimi,
wanafukizia ubani miungu ya uongo.
Wamejikwaa katika njia zao,
katika barabara za zamani.
Wanapitia vichochoroni badala ya njia kuu.
16Wameifanya nchi yao kuwa kitisho,
kitu cha kuzomewa daima.
Kila mtu apitaye huko hushangaa
na kutikisa kichwa chake.
17Nitawatawanya mbele ya adui,
kama upepo utokao mashariki.
Nitawapa kisogo badala ya kuwaonesha uso wangu
siku hiyo ya kupata maafa yao.”
18Kisha, watu wakasema: “Njoni tumfanyie Yeremia njama, maana hatukosi makuhani wa kutufundisha, wenye hekima wa kutushauri na manabii wa kututangazia ujumbe wa Mungu! Njoni tumshtaki kwa maneno yake mwenyewe, wala tusiyatilie maanani yote asemayo.”
19Basi, mimi nikasali:
Nitegee sikio ee Mwenyezi-Mungu,
usikilize ombi langu.18:19 usikilize ombi langu: Au sikiliza dua langu.
20Je, mtu hulipwa mabaya kwa mema?
Walakini, wamenichimbia shimo.
Kumbuka nilivyosimama mbele yako,
nikasema mema kwa ajili yao,
ili kuiepusha hasira yako mbali nao.
21Kwa hiyo waache watoto wao wafe njaa,
waache wafe vitani kwa upanga.
Wake zao wawe tasa na wajane.
Waume zao wafe kwa maradhi mabaya
na vijana wao wachinjwe kwa upanga vitani.
22Kilio na kisikike majumbani mwao,
unapowaletea kundi la wanyanganyi ghafla.
Maana wamechimba shimo waninase;
wameitegea mitego miguu yangu.
23Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu,
wazijua njama zao zote za kuniua.
Usiwasamehe uovu wao,
wala kufuta dhambi zao.
Waanguke chini mbele yako;
uwakabili wakati wa hasira yako.
Yeremia18;1-23
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.